1 Corinthians 4

Mawakili Wa Siri Za Mungu

1 aBasi, watu na watuhesabu sisi kuwa tu watumishi wa Al-Masihi na mawakili wa siri za Mungu. 2 bTena, litakiwalo ni mawakili waonekane kuwa waaminifu. 3Lakini kwangu mimi ni jambo dogo sana kwamba nihukumiwe na ninyi au na mahakama yoyote ya kibinadamu. Naam, hata mimi mwenyewe sijihukumu. 4 cDhamiri yangu ni safi, lakini hilo halinihesabii kuwa asiye na hatia. Bwana ndiye anihukumuye. 5 dKwa hiyo msihukumu jambo lolote kabla ya wakati wake. Ngojeni mpaka Bwana atakapokuja. Yeye atayaleta nuruni mambo yale yaliyofichwa gizani, na kuweka wazi nia za mioyo ya wanadamu. Wakati huo kila mmoja atapokea sifa anayostahili kutoka kwa Mungu.

6 eBasi ndugu zangu, mambo haya nimeyafanya kwangu binafsi na Apolo kwa faida yenu, ili mweze kujifunza kutoka kwetu maana ya ule usemi usemao, “Msivuke zaidi ya yale yaliyoandikwa.” Hivyo hamtajivunia mtu fulani na kumdharau mwingine. 7 fKwa maana ni nani aliyewafanya kuwa tofauti na wengine? Ni nini mlicho nacho ambacho hamkupokea? Nanyi kama mlipokea, kwa nini mnajivuna kama vile hamkupokea?

8 gSasa tayari mnayo yale yote mnayohitaji! Tayari mmekwisha kuwa matajiri! Mmekuwa wafalme, tena bila sisi! Laiti mngekuwa wafalme kweli ili na sisi tupate kuwa wafalme pamoja nanyi! 9 hKwa maana ninaona kwamba Mungu ametuweka sisi mitume katika nafasi ya mwisho kabisa, kama watu waliohukumiwa kufa kwenye uwanja wa tamasha, kwa sababu tumefanywa kuwa maonyesho kwa ulimwengu wote, kwa malaika na kwa wanadamu pia. 10 iKwa ajili ya Al-Masihi sisi ni wajinga, lakini ninyi mna hekima sana ndani ya Al-Masihi. Sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu. Tunadharauliwa, lakini ninyi mnaheshimiwa. 11 jMpaka saa hii tuna njaa na kiu, tu uchi, tumepigwa na hatuna makao. 12 kTunafanya kazi kwa bidii kwa mikono yetu wenyewe. Tunapolaaniwa, tunabariki, tunapoteswa, tunastahimili, 13 ltunaposingiziwa, tunajibu kwa upole. Mpaka sasa tumekuwa kama takataka ya dunia na uchafu wa ulimwengu.

14 mSiwaandikii mambo haya ili kuwaaibisha, bali ili kuwaonya, kama wanangu wapendwa. 15 nHata kama mnao walimu 10,000 katika Al-Masihi, lakini hamna baba wengi. Mimi nilikuwa baba yenu katika Al-Masihi Isa kwa kuwaletea Injili. 16 oBasi nawasihi igeni mfano wangu. 17 pKwa sababu hii ninamtuma Timotheo, mwanangu mpendwa na mwaminifu katika Bwana. Yeye atawakumbusha kuhusu njia za maisha yangu katika Al-Masihi Isa, ambayo yanakubaliana na mafundisho yangu ninayofundisha katika kila kanisa.

18 qBaadhi yenu mmekuwa na jeuri mkidhani kuwa sitafika kwenu. 19 rLakini kama Bwana akipenda, nitafika kwenu mapema, nami nitapenda kujua, si tu kile wanachosema hawa watu jeuri, bali pia kujua nguvu yao. 20 sKwa kuwa Ufalme wa Mungu si maneno matupu tu bali ni nguvu. 21 tNinyi amueni. Je, nije kwenu na fimbo, au nije kwa upendo na kwa roho ya upole?
Copyright information for SwhKC